Wabunifu VETA wapata ufadhili wa milioni 85 kutoka COSTECH

Wabunifu wa Ufundi Stadi, chini ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo  ya Ufundi Stadi (VETA), wamepata ufadhili wa jumla ya Shilingi 85  milioni kutoka kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa  ajili ya kuendeleza ubunifu wao.

Mkataba kwa ajili ya ufadhili huo umesainiwa jana tarehe 3 Juni  2019 katika ofisi za COSTECH jijini Dar es Salaam, kati ya Mkurugenzi  Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt.  Amos Nungu.

Ubunifu utakaopatiwa ruzuku ni “Pikipiki Salama” ya Mwl. Aneth  Mganga wa Chuo cha VETA Kipawa, “Mashine ya Kufukuza Ndege Waharibifu  Mashambani” ya Mwl. Emmanuel Bukuku wa Chuo cha VETA Dar es Salaam  (Chang’ombe) na “Kifaa cha Kufundishia Elimu ya Mfumo wa Jua na Sayansi  ya Anga” cha Ndg. Ernest Maranya, Mbunifu na Mhitimu wa Chuo cha VETA  Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt.  Pancras Bujulu, amesema VETA imebeba jukumu la kuwasimamia na  kuwadhamini wabunifu hao na kwamba Mamlaka hiyo itahakikisha ubunifu huo  unakamilika na kuingia sokoni kutatua changamoto mbalimbali  zinazoikabili jamii.

Baada ya kupokea ufadhili huo, mmoja wa wabunifu hao, Mwl. Emmanuel  Bukuku, amesema kuwa anaamini ruzuku hiyo itamsaidia kuboresha ubunifu  wake na kuhakikisha kifaa chake cha kufukuza ndege waharibifu mashambani  kinaingia sokoni na kuwasaidia wakulima kulinda mazao yao mashambani na  hatimaye kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.

Naye Mwl Aneth Mganga alisema kuwa ruzuku hiyo imekuja wakati  mwafaka ambapo anatamani kuboresha ubunifu wake wa “Pikipiki Salama” ili  kusaidia kupunguza athari za ajali za barabarani kwa watumiaji wa  pikipiki na wizi wa pikipiki, hasa zile zinazotoa huduma ya usafiri wa  kibiashara (maarufu kama bodaboda). Ajali hizo zimekuwa zikisababisha  vifo au ulemavu kwa vijana wengi nchini.

Kwa upande wake Ndg. Ernest Maranya ameishukuru COSTECH na VETA na  kusema kuwa ruzuku hiyo itamsaidia kwa kiasi kikubwa kufanya maboresho  muhimu kwenye kifaa chake na kutatua changamoto iliyokuwa ikimkabili ya  gharama za uagizaji wa malighafi nje ya nchi iliyosababishwa na ufinyu  wa fedha.

 Amesema kuwa kifaa hicho kikikamilika kitakuwa msaada mkubwa  katika kufundisha elimu ya mfumo wa jua na sayansi ya anga, hasa kwa  elimu ya msingi na sekondari. Ametoa wito kwa wabunifu wengine  kujitokeza na kusajili bunifu zao ili wale watakaokidhi vigezo waweze  kunufaika na ufadhili kama huo wa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia  COSTECH.