TANZANIA COMMISSION FOR SCIENCE AND TECHNOLOGY
(COSTECH)

News

Zaidi ya shilingi bilioni 9 zimetolewa na serikali ya Norway ili kusaidia tafiti za mabadiliko ya tabia nchi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira,  Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) amesema zaidi ya shilingi bilioni 9 zimetolewa na serikali ya Norway ili kusaidia tafiti za mabadiliko ya tabia nchi wakati akizindua programu wezeshi ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi , tarehe 11 Oktoba 2023, ukumbi wa COSTECH uliopo (Sayansi), kijitonyama - Jijini Dar es Salaam 

" Mwezi Septemba 2023 Serikali ya Tanzania ilisaini tena mkataba na Serikali ya Norway ili kuimarisha shughuli za maendeleo nchini kupitia ushirikiano katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi. Aidha, leo hii Tanzania imepata fedha, niwapongeze COSTECH kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutafuta fedha pamoja na Serikali zote za Norway na Swideni kuwezesha hilo hususani kukuza ushirikiano wa Tafiti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi " alisema Mhe. Dkt. Jafo

Mhe. Dkt. Jafo aliongeza kuwa, Tanzania ilijiwekea malengo ya kupunguza gesi hatarishi katika anga kwa kiwango cha asilimia 30 mpaka asilimia 35 hadi kufikia mwaka 2030 ili kupambana na mabadiliko ya Tabianchi. 


Aidha, Mhe. Jafo alipongeza Serikali ya Norway kwa kukubali kuingiza fedha kiasi cha zaidi ya Bilioni tisa (9) ili kugharamia Tafiti pamoja na Serikali ya Swideni kukubali kuongeza fedha inayolandana na kiwango kulichotolewa na Serikali ya Norway. 

" Ajenda ya Tafiti nchini itakuwa kubwa sana na COSTECH kama Taasisi yenye dhamana itapiga hatua kubwa yakupata tafiti zinazojibu changamoto za mabadiliko ya Tabianchi kwa Taifa letu" alisisitiza.

"Nikiwa kama Waziri mwenye dhamana ya mazingira,  naomba kushukuru wadau wote waliojitokeza leo kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daktari Samia Suluhu Hassan, yeye ni mwana mazingira na miongoni mwa jopo la watu muhimu waliochaguliwa kusimamia mazingira duniani" Alihitimisha mhe. Dkt Jafo