TANZANIA COMMISSION FOR SCIENCE AND TECHNOLOGY

MHE. KIPANGA; SERIKALI KUFANYA MAPITIO YA SHERIA NAMBA 7 YA COSTECH

Published at: Wed, Jul 13, 2022 1:20 PM

MHE. KIPANGA; SERIKALI KUFANYA MAPITIO YA SHERIA NAMBA 7 YA COSTECH

 Dar es salaam

Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia (WyEST) inatarajia kuanza mchakato wa mapitio ya Sheria Namba 7 ya mwaka 1986 ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili iendane na wakati wa sasa na kasi  ya Maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika kuchangia maendeleo ya Nchi.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Julai 11, 2022 na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia (WySTE), Mhe. Mhandisi Omary J. Kipanga ambaye alimuwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alipotembelea Banda la COSTECH katika Maonesho ya Kimataifa ya 46 ya Biashara Dar es salaam, maarufu kama Sabasaba.

Akizungumza baada ya kutembelea na kujionea bunifu mbalimbali zenye tija kutoka kwa vijana wa Kitanzania katika Banda hilo kwa Ufadhili wa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Mhe. Kipanga amesema kuwa, Sheria namba ya 7 ya mwaka 1986 ya  COSTECH, hatimaye kusimikwa rasmi mwaka 1988 hakukua na kipengele cha ubunifu ndani yake. Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa maagizo ya kupitia Sheria hiyo na Kanuni, na sera zake ili kuendana na mahitaji ya wakati wa sasa.

" Kwenye nyanja ya Ubunifu Taifa la Tanzania limepiga hatua kubwa.  Kwa sasa tunatengeneza bidhaa mbalimbali kupitia bunifu za ndani  hivyo nasisitiza bunifu hizi zilindwe kisheria ili watafiti na wabunifu wapate stahiki zao na ziwafaidishe wao binafsi na pia zisaidie kutengeneza ajira kwa wengine" amesema Naibu Waziri Kipanga.

Aidha, Mhe. Kipanga ameitaka COSTECH kuendelea kutafuta fursa na kutatua changamoto kwa  kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuendelea kulijenga Taifa kupitia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

" Lengo la bunifu hizi za ndani ni kutatua changamoto mbalimbali Nchini kwa sababu changamoto zinatofautiana kutoka Taifa moja hadi jingine, hivyo tutatumia bunifu zetu za ndani kutatua changamoto zetu" Naibu Waziri aliongeza.

COSTECH ni miongoni mwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia (WyEST). Kwa hiyo, "Nimekuja hapa kwa niaba ya Mhe. Waziri na nimeshuhudia mambo mazuri na yenye tija katika Taifa letu, Hongereni sana. Songeni mbele, Serikali ya Mhe Rais Mama Samia Suluhu iko pamoja nanyi”. Naibu Waziri aliongeza.  Naibu waziri ametembelea Watafiti na Wabunifu katika Banda la COSTECH na kuona  utaratibu wa uratibu, uhamasishaji na ukuzaji wa tafiti na Ubunifu na pia kuona bunifu na wabunifu mbalimbali ambao wamelelewa na COSTECH.

Amesema kuwa  Tume ina Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) kwa ajili ya kugharamia shughuli za utafiti na Ubunifu pamoja na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) ambayo huratibiwa ili  kuhakikisha tafiti na bunifu zinalelewa, kukuzwa na kuendelezwa ili zifikie hatua ya ubiasharishaji wa kuwa bidhaa ambazo zitatatua changamoto katika Jamii.

 

MATUKIO KATIKA PICHA

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary J Kipanga  akisaini kitabu cha wageni  mara baada ya kuwasili Banda la Tume ya  Taifa  ya  Sayansi  na  Teknolojia  (COSTECH) kujionea shughuli za Utafiti na Ubunifu katika Maonesho ya  46 ya Kimataifa ya Biashara Dar es salaam maarufu kama Sabasaba- Jijini Dar es  salaam.

 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary J Kipanga (mwenye suti nyeusi) akitazama teknolojia mpya ya mbegu  ya Nanasi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI, Mikocheni)  kwa Mtafiti Bi. Magreth Lupembe (wa kwanza kulia) mara baada ya kuwasili katika Banda la Tume ya  Taifa  ya  Sayansi  na  Teknolojia  (COSTECH)  katika Maonesho ya  46 ya Kimataifa ya Biashara Dar es salaam maarufu kama Sabasaba- Jijini Dar es  salaam.

Naibu Waziri wa Elimu , Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary J Kipanga (kulia) akitazama Teknolojia ya “Activated Carbon” inayozalishwa kutokana na vifuu vitokanavyo na nazi kutoka kwa mbunifu Zagalo Emmanuel mara baada ya kuwasili katika Banda la Tume ya  Taifa  ya  Sayansi  na  Teknolojia  (COSTECH)  katika Maonesho ya  46 ya Kimataifa ya Biashara Dar es salaam maarufu kama Sabasaba- Jijini Dar es  salaam.