TANZANIA COMMISSION FOR SCIENCE AND TECHNOLOGY

COSTECH YASHIRIKI UZINDUZI WA SAHARA SPARKS.

Published at: Thu, Oct 27, 2022 4:37 PM

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imeshiriki uzinduzi wa Kongamano la Sahara Sparks lililoandaliwa na Sahara Ventures na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo COSTECH. Kongamano la mwaka huu lilikuwa na kauli mbiu ya Uwezekano kufunguliwa (Potential unleashed). 

 Wadau wengine waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na UNDP kupitia mradi wa Funguo pamoja na Clouds Media group ambapo uzinduzi huo umefanyika Oktoba 17, 2022 katika ofisi za Sahara Ventures zilizopo Victoria, jijini Dar es salaam.

 Akizindua kongamano hilo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike, amesema kampuni hiyo tanzu ya Sahara Sparks ambayo imeandaa kongamano la vijana wabunifu na wote wenye hamasa na masuala ya teknolojia na ujasiriamali, imekuwa ikifanya hivyo kwa muda wa zaidi ya miaka saba.

 "Kwa takribani miaka saba Sahara Ventures imekuwa ikiandaa kongamano la Sahara Sparks ambalo limekuwa ikionesha njia ya kuleta pamoja vijana wenye mawazo ya kibunifu na watunga sera ili kuweza kujadili kwa namna gani ubunifu, teknolojia na ujasiriamali vinaweza kuwa chachu ya kuchangia maendeleo ya taifa la Tanzania.”

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt Amos Nungu, alisema kuwa COSTECH imeshiriki katika kongamano hilo kama mdau mkuu anayehusika na kuratibu na kuhamasisha masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu hapa nchini, na hivyo, kwa kuwa kongamano hili linahusu masuala ya ubunifu, ni wajibu wa COSTECH kushiriki ili kukutana na kubadilishana mawazo na wadau wengine wanaohusika na masuala haya.

“Tupo katika uzinduzi wa kongamano la Sahara Sparks kama wadau muhimu wanahusika na kuratibu na kuhamasisha masuala ya sayansi na teknolojia nchini. Ushiriki wetu katika kongamano hili ni pamoja na kukutana na kubadilishana mawazo na wadau wengine wanaohusika na masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu.”

Vilevile, Dkt. Nungu alibainisha kwamba COSTECH imekuwa ikiwasaidia vijana kupitia kumbi za ubunifu na atamizi ambazo zipo katika kanda na mikoa mbalimbali hapa nchini.

“Pia tunajivunia kuwa na miundombinu wezeshi na mazingira yanayowafanya vijana kupata fursa ya kuonekana, kusikika na kubadilishana mawazo kupitia kumbi za ubunifu na atamizi zilizopo sehemu mbalimbali hapa nchini ambazo zinawawezeshga kupata fursa za kuendeleza mawazo na bunifu zao."

Akieleza kuhusu uwezeshaji wa wabunifu na wajasiriamali, Meneja mradi wa Funguo Bw. Joseph Manirakiza, alisema kwamba Funguo inajivunia kushirikiana na Sahara Sparks katika kuendelea kuunga mkono juhudi za uwezeshaji wa wabunifu na wajasiriamali katika kupata mitaji ya kuendeleza biashara zao.

“Mardi wa Funguo unajivunia kushirikiana na Sahara Sparks katika kuendeleza ubunifu hapa nchini. Tunawahimiza wale wote ambao wako mstari wa mbele kukuza vipaji vya wajasiriamali tuweze kuunganisha nguvu katika kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wetu.”

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt Amos Nungu akiongea na vyombo vya habari wakati wa uzinduzi wa kongamano la Sahara Sparks ilioandaliwa na Sahara Ventures