Wadau wa Elimu Watakiwa Kutumia Bunifu Mbalimbali ili Kutatua Changamoto Zinazoikabili Sekta ya Elimu Nchini

Tume  ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imewakutanisha wabunifu  mbali mbali wa zana za kufundishia masomo ya sayansi na wadau wa Elimu  nchini. Kongamano hili lilofanyika katika ofisi za Taasisi ya Elimu  nchini (TAE) lilikuwa na lengo la kutatua changamoto mbali mbali ili  kuwezesha utumiaji wa bunifu zilizo buniwa kwa lengo la kurahisisha  ufundishaji wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari hapa nchini.

Akizindua  Kongamano hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa Dkt.  Philbert Luhunga alielezea umuhimu wa matumizi ya bunifu hasa kwenye  sekta ya elimu. Dkt Luhunga aliwakaribisha washiriki na kuwasisitiza  kutatua changamoto zinazo sababisha kutokutumika kwa bunifu mbalimbali  zilizo buniwa na wabunifu wa hapa nchini. "Ubunifu wowote unakuwa na  tija unapotumika kutatua changamoto katika jamii, hivyo angalieni namna  bora ya kutumia bunifu hizi zenye lengo la kutatua changamoto kwenye  sekta ya Elimu" alishauri Dkt. Luhunga.

Kongamano  hilo lilihudhuriwa na wadau mbali mbali kutoka sekta ya Elimu wakiwamo  wawakilishi kutoka Taasisi ya HAKIELIMU, SHULE DIRECT, Shirika la umoja  wa mataifa linalojihusisha na maswala ya Sayansi (UNESCO)-Tanzania, Chuo  Kikuu cha Dar es Salaam, na Mamlaka ya Elimu Tanzania.

Katika  Kongamano hilo bunifu mbali mbali za kufundishia masomo ya sayansi  ziliwasilishwa na kujadiliwa, baadhi ya bunifu hizo ni pamoja na ubunifu  wa SmartDarasa. Ubunifu huu unatumia njia za kieletroniniki na unaweza  kutumika kumfundisha mwanafunzi masomo ya sayansi kwa urahisi zaidi na  mwanafunzi kuelewa anachofundishwa kwa urahisi na wepesi zaidi. Ubunifu  mwingine uliowasilishwa unaitwa Jenga-Hub. Huu unajikita kuelimisha  watoto wenye umri wa kati ya miaka 7 mpaka 12  ili wawe na mawazo ya  kibunifu kwa lengo la kuwafanya kuwa wabunifu wa bunifu zenye tija hapo  baadae. 


Bunifu  nyingine zilizo wasilishwa ni pamoja na kifaa cha kieletroniki  kinachomwezesha mwanafunzi kujifunza kwa vitendo mzunguko wa kupatwa kwa  jua na mwezi kinachoitwa solar system electronics, ubunifu wa kutambua  uwezo wa kosa na kujifunza kwa kutumia kifaa cha kutoa sauti maalumu na  kifaa cha kufundishia mitaala ya elimu ya anga (Jua, Mwezi, Sayari na  Vimondo)

Bunifu zote hizo zilifadhiriwa na COSTECH kupitia mradi wa kukuza ubunifu (HDIF).

Akihitimisha  Kongamano hilo mwakilishi wa kamishna wa wizara ya Elimu alitoa  shukrani kwa COSTECH kwa kudhamini kongamano hilo na pia aliwasihi  wabunifu waendelee kushirikiana na wadau ili kuboresha eneo la  teknolojia na maudhui yanayoakisi elimu kwa vitendo nchini.


Washiriki    wa kongamano lililowakutanisha wadau mbalimbali  wa elimu na wabunifu   wa  zana za kufundishia masomo ya sayansi wakiwa  katika picha ya  pamoja   11/6/2020, Kinondoni, Dar es salaam.

Imetolewa na Afisa Uhusiano, 

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)