Wadau wa Viwanda na Vyuo Vikuu Nchini wakutana Kujadili Mahusiano Yatakayoleta Tija katika Mageuzi ya Uchumi wa Viwanda Nchini

Tume  ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH imeendesha Mdahalo kati ya  wadau wa Viwanda na Vyuo Vikuu ili kujadili kwa pamoja changamoto  zinazojitokeza katika eneo la mahusiano ili kuboresha mitaala ya elimu  na kujadili njia za kutatua changamoto na kuongeza kuongeza tija na  ufanisi pamoja na kasi ya uzalishaji wa ukuaji wa sekta ya viwanda  nchini.

Mdahalo  huo ulifunguliwa na Prof. Maulid Mwatawala Mwakilishi wa Makamu wa  Chuo cha Kilimo SUA, kwa kuwakaribisha wadau wote na amewataka  kuhakikisha wanaweka mikakati bora ya mahusiano ya pamoja ili kuendana  na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi kwa kuangalia  urasmishaji na  uhawilishaji wa Teknolojia kwa mandeleo ya viwanda nchini. Vilevile  kuangalia teknolojia zinazoakisi mazingira halisia ya nchi katika  kuongeza ushindani wa soko la ajira na umahiri wa wanafunzi/wahitimu  kukidhi mahitaji ya ukuaji wa sekta ya viwanda nchini. 


Wadau  mbalimbali waliojitokeza wakati wa ufunguzi wa mdahalo huo na  kuwasilisha mada mbalimbali na kujadili changamoto kwa pamoja ni  kutoka  Vyuo Vikuu nchini kikiwepo Chuo Kikuu Cha Kilimo SUA, kupitia (DPRTC)  ambayo ni Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhawawilishaji wa  Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu kupitia Kitengo cha “SUA Innovation  Hub” na Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Joseph- SJUIT kupitia idara ya ITAF,  Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT) na wadau wa Kongano (Cluster)  ya Mkoa wa Morogoro wanaofahamika kwa jina “Morogoro Food Processors  Clusters Initiative”


Aidha,  wawakilishi kutoka Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI)  inayosimamia  Sera na Ushawishi wa viwanda anaeleza ni muhimu kufanya tathimini ya  mahitaji “Training Need Assessment” ili kusaidia walimu na wanafunzi  kuendana na mazingira halisi. Kuahidi kuendelea kushirikiana na COSTECH  kama mshauri kwa kuwa kazi yao inategemea utafiti (Evidence based)  kuendesha shughuli zao.  Pia  Taasisi ya  wafanyabiashara wenye Viwanda, Biashara na Wakulima (TCCIA)  amesema  wanaendeleza mahusiano na Vyuo vikuu na viwanda kwa lengo la  kuwaunganisha ili  kuwapatia mafunzo kwa vitendo au uhalisia kwa kusudi la kukuza kada zao na uzoefu  wa ujasiriamali katika soko la ushindani la ndani na nje ya nchi. 


Akifunga  Mdahalo huu Dkt. Athumani Mgumia, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha  Uhawishaji wa Teknolojia (CDTT) ambae pia ni muwakilishi wa Mkurugenzi  Mkuu wa COSTECH amewashukuru wadau kwa kujitokeza na kujadili kwa pamoja  changamoto mbalimbali zinazojitokeza na amekaribisha mawazo yanayolenga  kufanya maboresho na kutoa mchango chanya kwa maendeleo endelevu ya  viwanda nchini.

Mdahalo  huu umeandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa  kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Taasisi.

Picha  ya Pamoja ya Washiriki wa Mdahalo wa Ubunifu na uboreshaji wa mahusiano  kati ya Vyuo vikuu na wadau wa Viwanda nchini. Siku ya Jumatano 17,  Juni 2020. Chuo Kikuu kilimo SUA, Mkoa wa Morogoro.


IMEANDALIWA NA;

AFISA UHUSIANO

TUME YA TAIFA YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA (COSTECH)