Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Kufanya Maboresho ya Mfumo wa Kusimamia Tafiti na Bunifu

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Amos Nungu amesisitiza ushiriki wa pamoja kwa wataalamu wa ndani na kusema kwamba hiyo itasaidia kuboresha mfumo.

Hayo aliyasema wakati akifungua Kikao cha Kikosikazi cha Maboresho ya Mfumo wa kielektroniki wa  Utafiti na Ubunifu jana katika ukumbi wa mkutano wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo iliyoko Mikocheni (MARI),  jijini Dar es Salaam.

Dkt. Nungu alisema kutokana na hilo hawana budi kujitahidi kwenda na wakati ili wanapomaliza maboresho ya mfumo wao kusitokee matatizo ya kimfumo hapo baadaye.

Akielezea katika kikao hicho Meneja wa Kitengo cha TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Ndugu Emmanuel Nnko amesema tupo katika jitihada za maboresho ya mfumo wa ndani ambao utasaidia kuiwezesha Tume kusimamia na kudhibiti utaratibu mzima wa utafiti na ubunifu katika maeneo mawili, kwanza ni kutoa vibali vya miradi ya utafiti na pili kutoa ufadhili kwa wabunifu.

Vilevile amesema kwasasa wataalamu wapo katika sehemu ya awali ya ukusanyaji wa mahitaji kutoka kwa watumiaji ili kuhakikisha mahitaji yote yanaingizwa kwenye mfumo na sehemu ya pili ni maendeleo ya mfumo ya kufanikisha mahitaji hayo.

Katika Kikao hicho washiriki walioshiriki mpaka sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Wakurugenzi wa Idara mbalimbali ikiwemo Kituo cha Kuendeleza na Kuhawilisha Teknolojia (CDTT), Kurugenzi ya Uratibu na Uendelezaji wa Utafiti (DRCP) na Kurugenzi ya Menejimenti ya Maarifa (DKM) pamoja na wadau kutoka taasisi nyingine kama TANESCO na NIDA ili kufanya maboresho ya Mfumo wa Tafiti na Ubunifu.

                             Wafanyakazi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia na wataalamu kutoka NIDA katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha kuboresha mfumo wa kusimamia Tafiti na bunifu