Watafiti Waahidi Kukamilisha Miongozo ya Kamati za Kusimamia Maadili ya Tafiti Katika Taasisi Zao

Watafiti kutoka katika Taasisi za tafiti nchini ambazo ni Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Taasisi ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) waahidi kukamilisha miongozo ya kamati za kusimamia maadili ya utafiti katika taasisi zao.

Watafiti hao wameyasema hayo mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu alipokuwa akifungua kikao Kazi cha kuandaa miongozo ya Kamati za kusimamia maadili ya Utafiti. Kikao hicho kinachofanyika katika ukumbi wa Wakala wa Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo na kimeandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) chini ya Kurugenzi ya Uratibu na Uendelezaji wa Utafiti (DRCP).

Akifungua kikao kazi hicho Dkt. A. Nungu alisema anatamani ifikapo mwezi wa Novemba mwaka huu wa 2020 amualike Waziri kwaajili ya kuzindua miongozo yetu kutoka katika taasisi zetu za utafiti ambazo ni TALIRI, TARI, TAFORI na TAFIRI.

Dkt. Nungu alisema, COSTECH inajitahidi kujenga uwezo katika taasisi za tafiti ili ziweze kusaidia kufanya kazi kwa urahisi zaidi.

Aidha kikao kazi hiki kina jumla ya wawakilishi kumi na sita (16) kutoka katika taasisi nne ambazo kila taasisi ilileta wawakilishi wanne (4) ili kushiriki kwa pamoja katika kikao kazi hicho cha kutengeneza miongozo ya kamati za kusimamia maadili ya utafiti.

Lengo la kikao kazi  hiki ni kuwajengea uwezo Taasisi zinazojishughulisha na tafiti nchini ili ziweze kufuata taratibu na kuzingatia miongozo ya kamati za maadili ya utafiti na hatimaye kutumia matokeo ya tafiti kujibu changamoto zinazojitokeza katika jamii yetu.

Washiriki mbalimbali walieleza jinsi wanavyotekeleza majukumu yao kisheria na kuonesha uhitaji wa kupata miongozo (Standard Operating Procedure) zitakazowaongoza ili kufanikisha shughuli za utafiti na kutengeneza kamati za maadili ya kusimamia utafiti katika Taasisi zao.

Dkt. Nungu aliwapongeza kwa Kazi nzuri inayoendelea kufanywa na wadau huku akisisitiza jukumu la kimsingi la utoaji wa vibali na kuwatakia kikao kazi chema chenye mafanikio.


Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha kuandaa Miongozo ya kamati za kuasimamia maadili ya utafiti yaliofanyika katika ukumbi wa Wakala wa Maendeleo Uongozi wa Elimu (ADEM) – Bagamoyo.