COSTECH Yashiriki Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Utafiti Kuhusu Mazingira

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeshiriki warsha ya kuhuisha Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Mazingira (NERA), inayosimamiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Kamati ya Ushauri wa Utafiti kuhusu Mazingira (ERAC).

Warsha hiyo imefanyika katika Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA) Mkoani Morogoro kuanzia tarehe 7 -8 Oktoba, 2020 ambapo washiriki wa Warsha hiyo ni wajumbe wa kamati kutoka katika Vyuo Vikuu, Sekta binafsi, Tawala za Mikoa na Taasisi mbalimbali zinazohusika na mazingira kutoka Tanzania Bara na Visiwani ambapo COSTECH ni mjumbe wa kamati hiyo.

Lengo la warsha hiyo ni kuzindua Kamati ya Ushauri wa Tafiti zinazohusu Mazingira pamoja na kuwapitisha wajumbe hao katika Ajenda ya Taifa ya Utafiti wa Mazingira 2017 – 2022 ili waweze kuifanyia maboresho.

Katika warsha hiyo, COSTECH iliwakilishwa na Bwana Merchades Rutechura ambaye aliwasilisha mada kuhusu “Nafasi ya Tume katika kuratibu na kuhamasisha tafiti zinazohusu Mazingira.”

Aidha, katika mawasilisho hayo, COSTECH iliainisha miradi ya utafiti na ubunifu iliyowahi kufadhiliwa kwa kipindi kilichoanzia mwaka 2015 – 2020; mafanikio yaliyopatikana; changamoto zinazoikumba Tume katika kuratibu na kuhamasisha tafiti zinazohusu Mazingira pamoja na njia inazotumia kutatua changamoto hizo.

Vilevile warsha hiyo iliambatana na uchaguzi wa Mwenyekiti wa ERAC ambapo Bw. Thomas Bwana kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, Idara ya Mazingira alichaguliwa kuongoza Kamati kwa kipindi cha miaka mitatu (3).

Warsha ilifunguliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Mhandisi Samuel Gwamaka Mafwenga.

Picha ya pamoja ya Wajumbe wa Kamati ya Ushauri wa Utafiti kuhusu  Mazingira kutoka Vyuo Vikuu, Sekta binafsi, Tawala za Mikoa na Taasisi  mbalimbali zinazohusika na mazingira kutoka Tanzania Bara na Visiwani.