COSTECH Yatoa Mafunzo Kwa Waandishi wa Habari Jinsi ya Kuandika Habari za Utafiti wa Sayansi

Tume ya Sayansi na Teknolojia COSTECH nimetoa mafunzo ya siku mbili kwa  waandishi wa habari  na watafiti jijini Dodoma  kwa lengo la kuwajengea uwezo namna ya kuandika habari za kisayansi ili ziweze  kuwafikia walaji kwa njia rahisi kwa kutumia wanahabari.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika Jijini Dodoma Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa kutoka COSTECH Dkt Philibert Luhunga amesema lengo ni kuona Teknolojia ya Sayansi inayobuniwa na Watafiti  inawafikia wananchi au walaji kwa lugha rahisi.

Alisema, Lengo la kuwakutanisha ni kutengeneza mahusiano mazuri baina ya waandishi na Watafiti ili kuwezesha  tafiti mbalimbali zinazofanywa na hawa watafiti ziwafikie wananchi kiurahisi kwa sababu tafiti hizo zinakuwa katika Lugha ya Sayansi, lakini tafiti hizo zikipelekwa kwa wananchi kwa kutumia wanahabari ni rahisi kueleweka na walaji wa tafiti hizo.

Aidha  Dkt. Luhunga amewataka waandishi wa habari kuandika mara kwa mara habari zinazohusu Sayansi hasa tafiti zinazofanywa na wataalamu wetu ili wananchi wanufanike na tafiti zinazofanywa na wataalamu wetu.

Alisisitiza hasa katika kipindi hiki nchi imejikita katika  uchumi wa viwanda Teknolojia za ndani ni muhimu sana katika maendeleo  ya Taifa ili kama nchi tufikie azma  ya kuwa nchi ya Viwanda.

Vilevile amesema  kuwa mpaka sasa  wameshafanya semina kama hizo katika Mikoa ya Dar es saalam, Tanga, Mtwara na Unguja na katika maeneo hayo kumeonekana matokeo chanya kwa waandishi kuwa na mwamko mkubwa wa kuripoti na kuandika habari za utafiti mbalimbali.

Alisema “Kote ambako tumefanya semina kama hizi kumeonyesha mwamko mkubwa sana wa kuripoti taarifa za sayansi na kitafiti zilizosaidia kuokoa maisha ya watu, hasa tafiti za hali ya hewa kwa kanda ya mashariki”.

Aidha amewashauri wananchi kuendelea kufuatilia habari za utafiti wa kisayansi katika nyanja mbalimbali na wasisite kuwasiliana na Mamlaka husika wanapoona mabadiliko ya kisayansi katika maeneo yao.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi  wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo  (TARI) Makutupora Dkt. Cornel Masawe amesema waandishi wa habari ni watu muhimu katika kufanikisha usambaaji wa tafiti za kisayansi ili  kuwafikia walengwa wa tafiti hizo.

Amesema kwa upande wa TARI wana takribani vituo kumi na saba (17) nchi nzima ambavyo vinafanya utafiti wa mbegu mbalimbali za mazao na wamekuwa wakizalisha teknolojia tofauti tofauti za mbegu za kilimo zinazoweza kuwanufaisha wakulima hapa nchini.

Alimalizia kwa kusema kuwa hapo mwanzo walikuwa wakitumia siku ya nane nane (Siku kuu ya wakulima nchini) ili kutangaza tafiti zao tukio lililokuwa likifanyika mara moja kwa mwaka lakini kwa sasa wamefungua ofisi katika kanda zote hapa nchini ambapo anaamini baada ya mafunzo haya waandishi wa habari wataminiminika kwenye ofisi zao kutaka kujua tafiti zinazofanywa.

Mafunzo haya yalifanyika katika ukumbi wa airport ambayo yameshirikisha washiriki arobaini (40) kati yao kumi na sita (16) walikuwa watafiti kutoka taasisi za utafiti na washiriki  ishirini na nne (24) walikuwa ni waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.Kaimu Mkurugenzi wa Menejiment ya Maarifa akifungua mafunzo ya watafiti na
Waandishi wa habari.


  

Mwezeshaji wa mafunzo ya watafiti na waandishi wa habari Dr. Dietrick Kaijanangoma
akisisitiza jambo kwa washiriki wakati akitoa mafunzo hayo.