Watafiti na Waandishi wa Habari Wakutanishwa Pamoja na Kujengewa Uwezo

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ndg. Ngusa Samike amehitimisha kilele cha mafunzo ya uandishi wa habari za kisayansi kwa kuwapatia vyeti washiriki wote 40 wakiwemo waandishi wa habari 25 pamoja na watafiti 15 kutoka mikoa ya kanda ya ziwa inayojumuisha Mwanza, Mara na Kagera.


Picha ya pamoja ya Mgeni wa heshima, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ndugu. Ngusa Samike (alieketi katikati pichani), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Philbert Luhunga (pichani kushoto), Msaidizi wa Katibu Tawala - Mwanza, Ndugu. Emily Kasagara(pichani  kulia) pamoja na watafiti  na waandishi wa habari kutoka kanda ya ziwa  mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo Jijini Mwanza.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa kwa siku mbili (2) kuanzia Jumanne ya Septemba 5, 2021 mpaka Jumatano ya Septemba 6, 2021 katika ukumbi wa mikutano ulipo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Jijini Mwanza.

Akihitimisha mafunzo hayo alisisitiza kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa kuwa yanatoa fursa kwa waandishi wa habari kushiriki kwa wingi katika kusambaza matokeo ya utafiti yaliyoko katika vyuo vikuu na vituo vya utafiti na maendeleo vilivyoko Kanda ya ziwa.

Ngusa aliwasisitiza waandishi kuhakikisha  wanachakata taarifa za matokeo ya utafiti na ubunifu ili yawafikie wananchi katika lugha rahisi na inayoweza kueleweka kwao.

"Kumekuwepo na dhana kwamba watafiti wanatumia lugha ngumu katika kuwasilisha matokeo ya tafiti wanazizifanya.  Nimejulishwa kwamba mafunzo haya yamewezesha watafiti kujikita katika kutumia msamiati rahisi wanapowasilisha matokeo ya tafiti zao. Nawasihi waandishi mtumie lugha rahisi ili

mlengwa wa kutumia matokeo haya, aweze kuyapata bila kigugumizi," alibainisha.

Alihitimisha kwa kuwashukuru Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kuratibu mafunzo haya yaliyowezesha kuwakutanisha pande zote mbili ili kuondoa dhana tofauti ambayo huwaathiri wananchi kwa kukosa taarifa sahihi.

" Nawapongeza COSTECH kwa jitihada hizi na naamini zitakuwa na manufaa kwa nyanja tofauti ikiwemo kilimo, mifugo, viwanda na sekta nyinginezo."

Mafunzo yaliyofanyika kwa waandishi na watafiti kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ni mwendelezo wa mafunzo yaliyowahi kufanyika mikoa ya Pwani, Morogoro, Tanga, Dar es salaam, Dodoma, Singida, Lindi, Mtwara, Unguja na Pemba.


Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ndg. Ngusa Samike akihitimisha mafunzo ya uandishi wa habari yaliyodumu kwa siku 2 kuanzia Septemba 5 - 6, 2021. Ukumbi wa Mikutano uliopo Ofisi za Mkuu wa Mkoa- Jijini Mwanza.MWISHO